Vigogo Nishati na Madini wapandishwa mahakamani
Vigogo wawili wa Wizara ya Madini na Nishati wamepandishwa kizimbani leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kosa la kuisababishia serikali hasara ya Shilingi bilioni 2.4 kwenye sakata la Almasi
Watuhumi hao ni pamoja na Mkurugenzi wa tathmini wa Wizara hiyo Archard Alphonce Karugendo na mthamini wa Serikali wa madini Edward Joseph Rweyemamu wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na kosa moja kila mmoja la uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya Shilingi Bilioni 2.4.
Wakisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage na wakili wa serikali Poul Kadushi ameiambia Mahakama kuwa, washtakiwa hao walitenda kosa hilo kati ya tarehe 25 na 31 mwezi wa nane mwaka 2017 katika maeneo ya mkoa wa Dar es Salaam na Shinganya nchini Tanzania.
Wakili Kadushi ameieleza Mahakama, walitenda kosa hilo wakiwa wathamini walioajiriwa na Wizara ya Nishati na Madini na kuongeza kwamba upelelezi dhidi kesi yao bado haujakamilika.
Wakili wa upande wa utetezi Nehemia Nkoko amedai mahakamani hapo kuwa wateja wake wanamuda mrefu tangu walipokamatwa hivyo kutaka upelelezi kukamilika haraka, huku wakili wa serikali akiambia Mahakama hiyo kuwa upelelezi utakamilika kwa wakati.
Washtakiwa hawakuruhusiwa kuzungumza chochote na kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 29 mwezi huu, huku watuhumiwa hao wakirejeshwa rumande, kutokana na kosa lao kutokuwa na dhamana.
Post a Comment