Sirro anataka kutuletea kizungumkuti - Kigaila
Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa CHADEMA, Benson Kigaila amefunguka na kutupa lawama kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Nyakoro Sirro na kusema kamanda huyo anataka kuleta kizungumkutu kutokana na kauli zake.
Kigaila amesema hayo leo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ambapo amesema jeshi la polisi halikuundwa kwa ajili ya kuwalinda viongozi tu bali liliundwa kwa lengo la kulinda wananchi na mali zao hivyo wanapaswa kuacha kuwatisha wananchi kuzungumza bali jukumu lao ni kuwalinda na kuwapa ulinzi wananchi.
"Tunataka kuwaambia polisi hao watu wanaojiita wasiojulikana sisi tunataka kuwasaidia kuwapata hao watu, polisi wanataka wazuie watu wasizungumze hii nchi ya Tanzania ni ya Watanzania Sirro anataka kutuletea kizungumkuti hapa, anasema anataka kupelekewa barua ya maombi ili aweze kufanya uchunguzi, hivi anapozuia mikutano ya chama cha siasa huwa anakuwa amepelekewa barua" alihoji Kigaila
Aidha Kigaila alisema kwa namna mambo yanayokwenda sasa nchini ni wazi kuwa usalama wa watu na mali zao ni mdogo sana na kusema hakuna mtu aliyesalama
"Mimi niwaambie kwa hatua ya sasa na uongozi huu hakuna mtu aliyesalama, lakini sisi tunajua majeshi, nguvu, kuteka na vitisho duniani kote havijawahi kushinda dhidi ya haki, tutakufa mmoja mmoja na tukifa damu yetu itazaa matunda yatakayozaa Demokrasia, walikufa Afrika Kusini, walikuwa Amerika, lakini lazima tuendelee kusema nchi hii ya kwetu sote hakuna mwenye hati miliki ya nchi hii, lazima viongozi wawe wasikivu na majeshi yalinde usalama wa raia na mali zao" alisema Kigaila
Mbali na hilo Kigaila amesema kuwa ni zaidi wa wabunge 11 wamelalamika kwa muda mrefu kuonekana kufuatiliwa na watu na magari lakini IGP, jeshi la polisi na watu wa usalama wamekuwa kimya kana kwamba wabunge hao hawajatoa malalamiko yao.
Post a Comment