Serikali yazifunga Bar

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mh. Reuben Mfune ameagiza bar zote, migahawa, vilabu vya pombe na grocery kufungwa kwa siku zisizojulikana kutokana na ugonjwa wa kipindupindu kuzidi kusambaa wilayani humo. 
Mkuu wa wilaya ametoa taarifa hiyo kupitia Afisa habari wa wilaya hiyo Daudi Nyingo na kuwataka wananchi kuwa makini na matumizi ya maji ya mito na mifereji kwani yameathiriwa na vijidudu vya kipindupindu. 
"Wananchi wote wa wilaya ya Mbarali mnatangaziwa kuwa hali ya ugonjwa wa Kipindupindu bado ni mbaya sana wilaya hapa, hivyo basi biashara zote za migahawa, vyakula vyote vinavyotembezwa, minada, vilabu vya pombe, bar, grocery zote, pamoja na mikusanyiko yote inayohusiana na sherehe, vyote vimefungwa hadi hapo mtakapotangaziwa tena" 
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali amesema kuwa mtu yoyote ambaye atakiuka maagizo hayo atachukuliwa hatua kali za kisheria
"Aidha mashine zote zitakazobainika kusaga vimea au unga wa pombe za kienyeji hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao Vilevile mnakumbushwa kwamba, maji yote ya mito pamoja na mifereji yameathiriwa na vijidudu vya Kipindupindu, hivyo basi wananchi wote mnaagizwa kuchemsha maji au kutumia vidonge vya 'water guard' pamoja na kufanya matumizi sahihi ya vyoo" alisema Mfune 
Hadi kufia Septemba 15, 2017 jumla ya wagonjwa 628 wamepatikana huku jumla ya watu nane wamefariki kutokana na ugonjwa wa Kipindupindu wilayani Mbarali jijini Mbeya.