Maisha wanayoishi Watanzania wanastahili - Waziri

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji amefunguka na kusema fedha nyingi zipo mikononi mwa wananchi kwani katika mzunguko wa fedha nchini zaidi ya asilimia 70 ya fedha zipo kwa wananchi huku asilimia 30 ya fedha ndiyo zipo kwenye mabenki.




Dk Ashatu Kijaji amesema hayo leo bungeni wakati akijibu swali kutoka kwa mbunge wa jimbo la Same Magharibi, Dk David Mathayo David na kusema kuwa mzunguko wa fedha mkubwa upo kwa wananchi na kusema wale ambao wanalalamika kuwa fedha hakuna ni kutokana na ukweli kwamba walikuwa wakikwepa kulipa kodi hivyo walikuwa na fedha nyingi zisizo zao ila kutokana na serikali kuwabana kwenye kodi hivyo maisha ambayo wanaishi sasa ndiyo maisha halisi. 
"Asilimia 30 tu ya fedha ndiyo iko benki na asilimia 70 ipo kwa wananchi kinachoonekana kwa sasa Naibu Spika ni kwamba serikali tumeimarisha mfumo wa ukasanyaji wa kodi, yule mfanyabishara ambaye alikuwa akifanya biashara bila kulipa kodi akijidanganya ile ni faida yake siyo ilivyo kwa sasa na tunaomba wabunge mtuunge mkono tuweze kukusanya kodi inavyostahili ili Watanzania sasa tuishi katika uchumi ambao taifa letu linastahili kuishi na wananchi wetu wanastahili kuishi, kiuhalisia fedha bado ipo mikononi ya kutosha mikononi mwa wananchi na uchumi wetu unaendelea vizuri" alisisitiza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji