Bunge lalipa fedha za matibabu ya Lissu
WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiulaumu uongozi wa Bunge kwa kukataa kukabidhi Sh milioni 43 za matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Bunge hilo limesisitiza kuwa limelipa fedha hizo Septemba 20, mwaka huu.
Lissu anaendelea na matibabu nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mkoani Dodoma, Septemba 7 mwaka huu. Jana Mbowe katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, aliulaumu uongozi wa Bunge na hasa akielekeza tuhuma zake kwa Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai kuwa wabunge wamekatwa posho kuchangia gharama za matibabu ya Lissu, lakini hadi jana hazikuwa zimekabidhiwa.
Hata hivyo, jana hiyo, Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ya Umma cha Bunge kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari, kukanusha tuhuma hizo kwa kusisitiza kuwa fedha hizo zimetumwa kwenye Akaunti Namba 0451155318 ya benki ya Barclays Tawi la Hurlringham, yenye jina la Kenya Hospital Association. Taarifa hiyo ilisema kuwa fedha hizo, zingeweza kutumwa mapema, lakini kulikuwa hakuna mawasiliano ya namna ya kupata akaunti ya kutumia fedha hizo.
Taarifa ilisema Bunge linatoa mwito kwa Watanzania wote, kuendelea kumuombea mbunge huyo apone haraka na kuendelea na shughuli zake za ujenzi wa nchi. Katika moja ya tuhuma zake kwa bunge hilo kuhusu fedha hizo, Mbowe alionesha kutokuwa na imani na Bunge kwa madai kuwa limeendelea kushikilia fedha hizo za Lissu wakati zinahitajika kwa matibabu. Pia Mbowe alijibu hoja iliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuwa serikali ipo tayari kugharamia matibabu ya Lissu katika nchi yoyote duniani, iwapo familia na madaktari wataridhia.
Mbowe alisema kuwa Chadema haina shida, iwapo familia ya Lissu itataka hivyo. Lakini, Mbowe alisema anaitaka serikali kutolichukulia suala hilo kiitikadi za kichama na kusiwe na nia ovu katika kumsaidia Lissu na kuwa ikibainika hivyo Chadema haitakubali. Mbowe aliweka bayana kuwa madaktari wamesema kuwa Mbunge huyo, hataweza kusafi rishwa nje ya nchi kwa matibabu kutokana na hali yake ya kiafya kutoruhusu misukosuko ya safari ndefu. Alisema hadi sasa Chadema imeshachangisha Sh milioni 204 kupitia michango mbalimbali kutoka kwa wananchi.
Alisema hadi kufi kia jana gharama za matibabu ya Mbunge huyo zilifi kia Sh milioni 162. Kwa mujibu wa Mbowe, Lisu ameshapitia awamu mbili za matibabu yake, ambapo ya kwanza ilikuwa ni katika Hospitali ya Dodoma na aliwapongeza madaktari kwa kumsaidia Lisu katika hatua ya awali. Alisema awamu ya pili ni madaktari sita wa Kenya, ambao wanaendelea kumtibu na kwa sasa afya inaimarika.
Alisema kuwa ataingia kwenye awamu ya tatu ya mazoezi, itakayochukua muda. Akizungumzia suala la uchunguzi wa Lisu, alisema hana wasiwasi na uwezo wa uchunguzi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya hapa nchini. Lakini, alisema ni vema serikali iruhusu vyombo vya ulinzi vya nje ya nchi, kama vile vya Marekani, Israeli, Ujerumani na Uingereza, kuja kuchunguza sakata hilo ili kujiridhisha zaidi. Mkutano huo wa Mbowe na waandishi, ulihudhuriwa na wabunge kadhaa - Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na viongozi wengine wa Chadema
Post a Comment