SHIRIKA la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limekabidhi vifaa vya radio kwa radio za jamii nne vyenye thamani ya mamilioni ya shilingi.
Unesco imesema kwamba utoaji wa vifaa hivyo umelenga kuongeza usikivu wa mawimbi ya radio katika maeneo ya vijijini.
Shughuli ya kukabidhiana imefanyika Agosti 17 mwaka huu.
Akizungumza wakati wakukabidhiana vifaa hivyo Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues alisema kwamba UNESCO inatambua kazi nzuri zinazofanywa na radio hizo za jamii za kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Aidha alisema ni muhimu sana kwa radio hizo za jamii kujiangalia na kujitunza zenyewe ili wasiingie katika matata na kuchapisha au kutangaza stori baada ya kukamilika kwake.
Alisema ipo haja kwa vyombo vya habari kufanyakazi kwa mujibu wa taratibu zao na kuhakikisha kwamba hawachapishi habari ambazo zinahatarisha uwapo wa uandishi unaozingatia maadili.
Meneja wa radio ya Jamii ya Baloha FM, Samada Maduhu aliishukuru UNESCO kwa kusaidia kituo chake na kwamba wanatarajia kufikia wilaya tano.
Alishukuru UNESCO kwa kuwawezesha kufika katika wilaya tano na kwamba kwa msaada huo wataokoa shilingi laki saba kwa mwezi kuazima transmita.
“Radio yetu inawafikia watu 500,000 lakini kwa kupatiwa hivi vifaa tutaweza kufikia watu milioni 1 katika wilaya zaidi ya tano za Kahama, Shinyanga Vijijini, Nyang’wale na Mbogwe mkoani Geita na pia Nzega na Uyui mkoani Tabora ,” alisema meneja huyo .
Kwa mujibu wa Maduhu, kama wasingelipata transmita hiyo wangelikuwa wanatumia sh milioni 8.4 kwa mwaka.
Kwa upande wake, Ayubu Kalufya wa radio ya jamii Uvinza alisema kwamba kituo chake kilikuwa kinakodisha transmita kwash laki tano na kufanya kwa mwaka mzima kutumia sh milioni 6.
Alisema kwa kupata vifaa hivyo walikuwa wanaachama na ukodishaji huo.
Kwa mujibu wa Kalufya, transmita hiyo mpya itawafikisha mbali zaidi katika pwani za Ziwa Tanganyika na hivyo kuleta mabadiliko yanayokusudiwa.
Kalufya alisema wananchi wakisikia mambo mbalimbali ya kuwaelimisha na wao wakapata nafasi ya kutoa maneno yao haki za binadamu zitakuwa zimeheshimiwa sana nchini.
Aliishukuru Unesco kwa kuendelea kuwasaidia na kusema kama si kwa msaada wa UNESCO jamii zilizopo pembezoni zisingepata nafasi ya kutoa madukuduku yao.
Radio nyingine zilizonufaika na msaada huo ni Pangani FM. Radio hiyo sasa inaweza kusikika Tanga nzima badala ya Pangani pekee.
Katika orodha ya redio zilizopatiwa vifaa ipo pia Mkoani FM ya kutoka Zanzibar.
Post a Comment