SERIKALI YAONGEZA UZALISHAJI KATIKA MAZAO MAKUU YA CHAKULA JAMBO LINALOPELEKEA KUJITOSHELEZA KWA CHAKULA NCHINI KWA ASILIMIA 100
Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe William Tate Ole Nasha (Mb) akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tizeba wakati wa uzinduzi wa maadhimisho
ya sikukuu ya wakulima - Nanenane, mwaka 2017 katika viwanja vya
maonesho ya kilimo ya Ngongo Mkoa wa lindi, jana tarehe 1/8/2017. (Picha zote na Mathias Canal)
Na Mathias Canal, Lindi
Serikali imeongeza uzalishaji katika
mazao makuu ya chakula hususani mahindi, mchele, mtama, uwele, na mikunde jambo
linalopelekea kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 100.
Aidha, Uzalishaji mwingine umeongezeka
kwenye mazao ya jamii ya mizizi kama muhogo, ndizi, viazi vitamu na mviringo.
Hayo yamesemwa jana tarehe 01/08/2017
na Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. Wiliam Tate Ole Nasha (Mb)
wakati akizungumza na wakulima wadau wa kilimo Mifugo na Uvuvi na wananchi kwa
ujumla wakati wa uzinduzi wa sikukuu ya wakulima – nane nane, Maonesho yenye
kauli mbiu ya “Zalisha kwa Tija Mazao na
Bidhaa za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati” yanayofanyika Kitaifa kwenye uwanja
wa maonesho ya kilimo wa Ngongo Mkoani Lindi.
Alisema kuwa Katika mwaka 2015/2016
Sekta ya Kilimo ilichangia asilimia 29.1 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na
asilimia 29.0 mwaka 2014/2015. Mchango mkubwa katika Pato la Taifa ulitokana na
Sekta ya Kilimo, ikifuatiwa na Sekta nyingine za kiuchumi.
Mchango huo mkubwa ni Kwa kuwa
asilimia kubwa ya Watanzania wanashiriki katika shughuli za kilimo, hivyo
kilimo kinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato na kupunguza umaskini.
Mhe Nasha Alisema kuwa uzalishaji wa
mazao, mifugo na uvuvi umeimarisha zaidi usalama wa chakula na lishe nchini, ambapo
katika mwaka 2015/2016 uzalishaji wa chakula ulikuwa ni tani milioni 16.2 ikiwa
ni ongezeko la tani milioni 0.7 (sawa na 4.5%)
ikilinganishwa na tani milioni 15.5 mwaka 2014/2015.
Uzalishaji wa mazao ya nafaka
umeongezeka kutoka tani milioni 8.9 mwaka 2014/ 2015 hadi tani milioni 9.5
mwaka 2015/ 2016 ikiwa ni ongezeko la tani milioni 0.6 (sawa na 6.7%). Uzalishaji wa mahindi umeongezeka kutoka tani
milioni 5.9 mwaka 2014/2015 hadi tani milioni 6.1 mwaka 2015/2016 sawa na
ongezeko la tani milioni 0.2 (sawa na 3.4%). Uzalishaji wa mchele uliongezeka
kutoka tani milioni 1.9 mwaka 2014/ 2015 hadi tani milioni 2.2 mwaka 2016 sawa
na ongezeko la tani milioni 0.3 (sawa na 15.8%).
Vilevile, uzalishaji wa mazao ya
chakula yasiyo nafaka umeongezeka hadi kufikia tani milioni 6.7 ikilinganishwa
na tani milioni 6.6 kwa mwaka 2014/ 2015 ikiwa ni sawa na ongezeko la tani
milioni 0.1 (sawa na 1.5%).
Kwa ujumla uzalishaji wa mazao ya
chakula ukilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.2 ya chakula na matumizi
mengineyo katika mwaka 2016/2017 unaonesha kuwepo kwa ziada ya tani milioni 3.0
za chakula. Kutokana na hali hiyo Taifa limejitosheleza kwa chakula kwa
asilimia 123 ambayo ni ongezeko la asilimia 3 ikilinganishwa na asilimia 120 ya
mwaka 2015.
Katika mwaka 2016/2017 idadi ya mifugo
nchini imefikia ng’ombe milioni 28.44, mbuzi milioni 16.67 na kondoo milioni
5.01. Pia, wapo kuku wa asili milioni 37.43, kuku wa kisasa milioni 34.5,
nguruwe milioni 1.85 na punda wapatao
572,357. jumla ya mitamba 634 ilizalishwa kutoka mashamba ya Serikali na
Kampuni ya Ranchi za Taifa - NARCO ikilinganishwa na mitamba 646 iliyozalishwa
mwaka 2015/2016. Aidha, jumla ya mitamba 10,820 ilizalishwa na Sekta binafsi na
kusambazwa kwa wafugaji wadogo nchini ikilinganishwa na mitamba 10,803
iliyozalishwa mwaka 2015/2016.
Mhe Nasha alisema kuwa Vituo vya Kanda
vimeendelea kuimarishwa kwa kupatiwa vitendeakazi, ukarabati wa miundombinu na mitambo ili
kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya uhimilishaji wakati wote.
Jumla ya dozi 100,000 za mbegu bora za
mifugo zilizalishwa ikilinganishwa na dozi 80,000 mwaka 2015/2016. Pia, ng’ombe waliohimilishwa
wameongezeka kutoka 221,390 mwaka
2015/2016 hadi ng’ombe 457,557 mwaka 2016/2017.
Post a Comment