RC TABORA –LIMINE ALIZETI KWA WINGI WAWEKEZAJI WALETE VIWANDA HAPA.
Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri ameagiza kuanzia msimu ujao wa
kilimo kila mtu mwenye uwezo wa kufanyakazi ni lazima alime heka mbili
za alizeti kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kujenga Viwanda vya kusindika
na kuzalisha mafuta hayo kuanza ujenzi mkoani humo.
Bw.
Mwanri alitoa kauli hiyo jana wakati wa ufunguzi wa maonesho ya
nanenane kwa Kanda ya mikoa ya Magharibi yaliyofanyika mkoani Tabora.
Alisema zao la alizeti katika mkoani Tabora
linastawi sana na ikiwa wakazi wake watalima kwa wingi Kampuni
mbalimbali zitajitokeza kwa wingi kuja kujenga viwanda vya kuzalisha
mafuta hayo.
Bw.Mwanri
alisisitiza kuwa wawekezaji wengi wamekuwa wanashindwa kuja kujenga
viwanda vya usindikaji wa mafuta hayo kwa sababu siku za nyuma zao hilo
limekuwa halitiliwi mkazo na kufanya uzalishaji kuwa wa chini sana ,
lakini hivi sasa hiyo itakuwa ajenda ya Mkoa kama mkakati mojawapo wa
kuwavutia watu kuja kujenga viwanda.
“Ndugu zangu Wakuu wote wa Wilaya na Wakurugenzi kuanzia sasa akili yetu na agenda yetu kubwa iko katika kuhakikisha kuwa kila mkazi wa Tabora analima heka
mbili za alizeti kuanzia msimu ujao wa kilimo ili tuwe na malighafi
nyingi kwa ajili ya kulisha viwanda vitakavyoanzishwa kwa mwaka mzima”
alisema Mkuu huyo Mkoa.
Katika
kutekeleza agizo hilo aliwaagiza Maafisa Ugani wote mkoani hapa
kuhakikisha wanawatembelea wakulima vijijini kwa ajili ya kuwaelimisha
juu ulimaji bora na mbegu bora za zao hilo kwa ajili kuwafanya wakulima
kuanza mara moja kilimo hicho pindi mvua za masika zitakapoanza.
Katika
hatua nyingine aliwaagiza Wakurugenzi Watendaji wote na Maofisa Ugani
wote kuhakikisha kuwa wanaanza wanawahimiza wakazi wa maeneo mbalimbali
ya Mkoa huo kuanza kilimo cha zao la uwele , mtama, viazi na mihogo ili
kukabiliana na tatizo la upungufu wa chakula kwa sababu ya mvua kuendelea kunyesha chini ya kiwango.
Alisema
tabia ya baadhi ya wananchi kuendelea kung’ang’ania mazao yanatumia
miezi mingi kukomaa kusababisha wakazi hao kuendelea kukabiliwa na
upungufu wa chakula wakati wakilima mazao yanayostahimili ukame tatizo haliwezi kuwapata.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Nzega alisema kuwa wao tayari wameshaanza maandalizi
kwa kuwa na shamba la mfano la heka 10 ambapo tayari wameshazalisha
alizeti na kutoa mafuta.
Alisema
kinachofuata ni kuongeza wigo wa kilimo hicho wa kuwashirikisha
wananachi wengi kwa kuwaelimisha juu ya kilimo bora cha zao hilo ili
waweze kuzalisha kwa wingi na kutoa fursa kwa wamiliki wa viwanda kupata
malighafi ya kutoa kwa ajili ya uzalishaji mafuta.
Naye Mkazi wa Ipuli mkoani Tabora Juma Elia aliunga mkono agizo la Mkuu wa Mkoa wa Tabora la kuhamasisha wakulima kuanza kulima alizeti ambalo ni rafiki na mazingira kwa sababu halihitaji kuni kukauka kama ilivyo tumbaku.
Aliongeza
kuwa zao hilo litasaidia kutoa ajira kwa njia ya vijana kushiriki
kilimo na wengine kuajiriwa katika viwanda vya kusindika mafuta ya
alizeti vitakavyoanzishwa.
Post a Comment