MAKONDA: TUNAITENGENEZA DAR MPYA

Posted on: August 16th, 2017
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo amekabidhiwa mradi wa Maboresho ya Mtaa Samora uliogharimu zaidi ya Shilingi Milioni 840 zilizofadhidhiliwa na  Serikali ya Japan kupitia Shirika la Kimataifa la maendeleo Japan (JAICA) na Manispaa ya Ilala uliokamilika kwa asilimia 100%.

Mradi huo umehusisha ujenzi wa sehemu za Maegesho, mapumziko ya watu,upandaji wa miti na Maua, maboresho ya mazingira, uwekaji wa alama za barabarani pamoja na maboresho ya mitaa kuanzia Makutano ya Barabara ya Samora na Morogoro ikienda sambamba na kupunguza msongamano.

Akizungumza kwenye makabidhiano hayo Mhe.  Makonda amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema kuhakikisha majengo yote ya Ghorofa eneo la Posta yanafungwa Taa na Runinga za Matangazo ili kupendezesha Mji na kuongeza mwanga nyakati za usiku.

Amesema katika nchi zilizoendelea ikiwemo Marekani majengo marefu yamekuwa sehemu ya matangazo hususani nyakati za usiku na kufanya miji kupendeza hivyo hata Dar es salaam tunaweza kufanya hivyo ili kufikia azma ya Rais Magufuli kutaka Dar es salaam kuwa mji wa Biashara.

Aidha amesema mradi huo utakuwa wa awamu ili kuhakikisha mitaa na maeneo ya wazi yanaboreshwa ilikuwafanya wananchi kuwa na maeneo mengi ya kupumzika na kubadilishana mawazo ikiwa ni maono yake ya Dar es salaam Mpya.

Awali eneo hilo lililofahamika kama Kaburi Moja lilikuwa likitumika kama Choo, Maegesho holela na wakati mwingine likitumiwa kwa uhalifu na uchafu wa mazingira.

Amewataka wananchi kutunza vizuri eneo hilo ili liweze kuwanufaisha wengi huku akipiga marufuku wamachinga kutofanya biashara kwenye eneo hilo.

 Aidha Makonda amesema anataka kuona vituo vyote vya Daladala mkoa wa Dar es salaam vinaboreshwe kuwa vya kisasa na kuwa sehemu ya matangazo ili kupendezesha mji na kuchangia ongezeko la mapato.