Jaji mkuu Kenya asema yuko tayari kwa kesi za baada ya uchaguzi
TANZANITE BLOG
Jaji mkuu wa Kenya, David Maraga, Alhamisi alisema kwamba majaji na
maafisa wengine wa mahakama za nchi hiyo wanaendelea kupokea mafunzo ya
ziada wakijitayarisha kusikiliza kesi ambazo huenda zikatokana na
uchaguzi utakaofanyika nchini humo wiki ijayo.
Malumbano ya hadharani yalindelea kushuhudiwa kati ya jaji huyo mkuu
na wanasiasa wa mirengo yote miliwili, licha ya Maraga kuwahakikishia
Wakenya kwamba mahakama ziko tayari kusikiliza na kutatua mizozo yoyote
itakayoibuka kufuatia uchaguzi wa Jumanne.
Haya yalijiri wakati jaji huyo anaendelea kukabiliwa na shinikizo
kutoka kwa wanasiasa, baadhi yao wakitaka majaji fulani kutosikiliza
kesi hizo, iwapo zitawasilishwa mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi, Maraga alisema
kwamba licha ya shutuma zinazotoka kwa baadhi ya Wakenya, mahakama hizo
zitafanya kazi usiku na mchana, na hata wikendi, ili kuzisikiliza kesi
za uchaguzi katika muda uliowekwa kikatiba.
"Kwa mujibu wa sheria, kesi hizi ni lazima zisikilizwe katika kipindi cha siku 14," alisema jaji Maraga.
Aidha Maraga alizindua kitabu cha kanuni wanazotakiwa kufuata majaji wakati wa kuamua kesi zinazohusu uchaguzi.
Haya yalijiri wakati ambapo idara ya mahakama imeendelea kupata
shinikizo kutoka kwa wadau mbali mbali, huku wengine wakiwataka baadhi
ya majaji kujiondoa kutoka kwa kesi ambazo huenda zitawasilishwa baada
ya uchaguzi na kusema kuwa wengine wana mnasaba na baadhi ya viongozi.
Siku ya Jumatano, jaji Maraga aliwataka wanasiasa kutoingilia masuala
ya utenda kazi wa mahakama na kuwataja viongozi wa kisiasa, wakiwemo
rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa chama cha ODM na mgombea wa urais wa
muungano wa NASA, Raila Odinga, pamoja na kiongozi wa walio wengi katika
bunge, Aden Duale, kama baadhi ya watu wanaoingilia shughuli za
mahakama kwa njia isiyofaa.
Pande zote mbili zimeelezea kutoridhika kwake na baadhi ya maamuzi ya
mahakama, hususan wakati kesi hazikuamriwa kama walivyopenda.
Na baada ya jaji mkuu kumsuta kiongozi wa wengi bungeni, siku ya
Alhamisi, mbunge wa Garissa mjini Aden Duale, ameendelea kulalamika
kwamba chama cha Jubilee hakina Imani na jaji wa mahakama kuu, George
Odunga.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha KTN akiwa mjini Garisa,
Duale alitaka jaji mkuu kumshinikisha jaji Odunga kujiondoa kwa kesi
zinazohusu uchaguzi kwani, kilingana na Duale, ana uhusiano wa karibu na
viongozi wa muungano wa NASA.
Lakini jaji mkuu wa Kenya ameshikilia kwamba hana mamlaka ya kumtaka jaji mwingine kujiondoa kutoka kwa kesi yoyote.
Haya yanajiri huku wagombea wakuu wa urais Uhuru Kenyatta, na Raila
Odinga,wakikita kambi katika maeneo mbalimbali kuwarai wapiga kura
kuwapa nafasi ya kuwahudumia kutoka ikulu.
Odinga na ujumbe wakla walikuwa katika Magharibi ya Kenya, huku
Kenyatta na wenzake wakifanya kampeni katika kaunti za Meru, Tharaka
Nithi na Kitui.
Imeandikwa na BMJ Muriithi akiwa Nairobi, Kenya.
Post a Comment