DC Ikungi aipa mbinu NMB jinsi ya kupata wateja wenye uwezo wa chini
TANZANITE BLOG
Mkuu wa
wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Miraji Mtaturu, ameyashauri mabenki
ikiwemo NMB kubuni bidhaa zitakazowanufaisha Watanzania wasio na uwezo
(maskini), ili kuondoa dhana inayowabaguzi ya ‘maskini sio rafiki wa
taasisi za kifedha’.
Mtaturu ametoa wito huo juzi wakati akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa tawi la NMB benki Ikungi.
Alisema
kuendelea kuamini kwamba maskini sio rafiki wa mabenki,kundi hilo la
Watanzania litaendelea kudidimia ndani ya lindi la umaskini.
“Kaeni
muangalie kundi hili la watu maskini litanufaikaje na huduma
zinazotolewa na mabenki ikiwemo ninyi NMB. Kundi hili la Watanzania
maskini ili liweze kujikomboa kiuchumi, basi mabenki badala ya kutoa
mikopo ya fedha taslimu, toeni mikopo ya mizinga ya nyuki, mabwawa ya
kufungia samaki au kuku kwa ajili ya kufunga kibiashara,” alishauri Mtaturu.
Akisisitiza,mkuu
huyo wa wilaya, alisema ili Mtanzania akiwemo maskini aweze kupata
maendekeo ya kweli ni lazima ajiongeze kwa kupata mikopo kutoka kwenye
taasisi za kifedha.
“NMB ninyi mnakwenda vizuri na
mnakwenda na wakati.Mmeendelea kubuni bidhaa/huduma mbalimbali ambazo
zimepelekea kuvutia Watanzania zaidi ya milioni mbili kufungua akaunti
kwenye matawi yenu nchini kote,” alisema na kuongeza.
“Sasa
mmebuni akaunti ya FANIKIWA,ambayo inawalenga wajasiriamali wadogo
wakiwemo baba/mama lishe na wauza chips, hongereni sana”.
Mtaturu
alisema sasa umefika wakati wa kuliangalia upya kundi la Watanzania
maskini, ili na lenyewe liweze kushiriki kikamilifu kuipeleka Tanzania
kwenye uchumi wa kati.
Aidha,
Mtaturu ametumia fursa hiyo kuwaalika wakazi wa wilaya ya Ikungi
wahakikishe wananufaika kikamilifu na huduma mbalimbali zinazotolewa na
tawi la NMB Ikungi.
“Najua wazi wakazi wengi wa wilaya yetu wameshindwa kunufaika na huduma za kibenki ikiwemo
mikopo, kutokana na benki zote kuwa Singida mjini umbali wa kilometa
45. Sasa NMB imesongeza huduma karibu, tuitumie fursa hii kwa kupata
mikopo kwa ajili ya kukuza mitaji na kupanua kilimo kikiwemo cha
alizeti,” alisema.
Katika
hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya huyo,ametumia nafasi hiyo
kuipongeza na kuishukuru benki ya NMB, kwa msaada wake wa vifaa tiba kwa
kituo cha afya Ikungi vyenye thamani ya shilingi milioni tano.
“Naagiza
vitanda hivi vitatu vya kujifungulia, vifaa vya kujifungulia, vitanda
na magodoro mawili ya kupumzikia wagonjwa na mizani mbili, vitunzwe
vizuri viweze kutumika kwa kipindi kirefu,” alisema.
Awali meneja
NMB kanda ya kati, Straton Chilongola, alisema msaada huo wa vifaa tiba
ni mwendelezo wa NMB kuunga mkono serikali ya awamu ya tano katika
kuboresha sekta ya afya.
Aidha, alisema benki hiyo imeendelea kubuni bidhaa mbalimbali na zenye kuzingatia mahitaji halisi ya soko kwa wakati husika.
“Moja
ya bidhaa hizo,ni kampeni ya ‘FANIKIWA’ akaunti ambayo ni mahususi
kabisa kwa wajasiriamali wadogo wadogo. Wajasiriamali hao ni pamoja na
baba/mama lishe, wauza chipis, wenye maduka ya biashara yakiwemo ya
nguo,” alifafanua Chilongola.
Akifafanua zaidi,alisema akaunti hiyo inampa fursa mteja kupata mkopo wa shilingi laki tano hadi shilingi 30 milioni.
Pia meneja huyo,alisema wanayo akaunti nyingine ya ‘Wajibu’ ambayo ni mahususi kwa ajili ya watoto wenye umri wa miaka 0-18.
“Kwa
upande wa teknolojia,tuna akaunti ya ‘Chap Chap’. Akaunti hii mteja
anaweza kufungua akaunti kwa muda mfupi na papo hapo kupata kadi yake ya
ATM, na kuanza kufanya miamala wo wote,” alisema Chilongola.
Benki
ya NMB, ina matawi zaidi ya 200 na mashine za kutolea fedha zaidi ya
700 nchi nzima.Ina wateja zaidi ya milioni mbili jambo linaloifanya kuwa
benki pekee nchini yenye hazina ya wateja wengi kuliko benki zingine
zilizopo nchini.
Post a Comment