Wananchi wa Sumbawanga Mkoani Rukwa Wamepinga kujengwa Kwa Kiwanda Cha Kusindika Nafaka.



Wakazi wa maeneo ya Mjimwema kata ya Malangali kwenye Manispaa ya Sumbawanga, wamepinga vikali ujenzi unaoendelea wa kiwanda cha kusindika nafaka, jirani kabisa na Zahanati ya Malangali hali itakayoathiri utendaji wa zahanati hiyo na afya za wagonjwa








Wananchi hao wa kata hiyo wakiongea mbele ya mbunge wa Sumbawanga mjini Mheshimiwa Aeshi Hilal, wamesema kiwanda hicho cha kusindika nafaka kikianza kufanya kazi, kitaathiri mno hali za wagonjwa wanaopata huduma kwenye zahanati hiyo, ikiwa pamoja na akina mama wajawazito wanaotegemea kujifungua katika zahanati hiyo

.
Kutokana na hali hiyo wananchi hao wamepinga vikali ujenzi wa kiwanda hicho na kusema haupaswi kuendelea katika eneo hilo

Akizungumza na wananchi hao mbunge wa Sumbawanga mjini Mheshimiwa Aeshi Hilal, amesema licha ya serikali ya awamu ya tano kuhimiza ujenzi wa viwanda nchini, lakini ujenzi huo ni lazima uzingatie sheria na taratibu zote za afya na mazingira kwa ujumla, na hasa ikizingatiwa kuwa manispaa hiyo imeshatenga tayari maeneo ya uendelezaji wa viwanda.