RC MAKONDA : KUBORESHA SEKTA YA AFYA KUTAPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO.
Posted on: July 25th, 2017
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Paul Makonda
leo ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa wodi ya kisasa ya
kinamama na watoto inayojengwa Hospital ya Amana yenye thamani ya
shilingi Billion 1.2 ambapo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia mia (100%).
Wodi hiyo ya kisasa itakuwa na uwezo wa kuchukuwa vitanda 150 ambapo
ndani yake kutakuwa na Vifaa vya kisasa vya kutolea huduma, Vyumba vya
Madaktari, vyoo vya kisasa ,mabomba ya maji, taa za kisasa na sehemu ya
kutosha ya wagonjwa kukaa wakati wakisubiri kuhudumiwa.
Ujenzi wa Wodi hiyo ni unafadhiliwa na Kampuni tanzu ya Mafuta na Saruji ya Amsons Group
ambayo imekubali kumuunga mkono Mheshimiwa Makonda kwa kujenga wodi
tatu wazazi na watoto kwenye Hospital za Amana, Temeke na Mwananyamala
ambapo zote zitakuwa na uwezo wa kuchukuwa vitanda 450.
“Ujenzi huu na hatua iliyofikia inatoa matumaini mapya
kwa kinamama, watoto na wakazi wa Dar es salaam juu ya upatikanaji wa
huduma bora na nzuri kwenye Hospital zetu za Serikali, watu walishazoea
huduma nzuri zinapatikana nje ya Hospital za Serikali lakini kwa sasa
hali itabadilika, na nina uhakika ndani ya muda mfupi tutamuomba Rais
Dr.Magufuli aje atuzindulie hizi wodi kama ishara ya kumbukumbu ya kazi
aliyoianza alipotembelea Hospital ya Muhimbili na kukuta watu wamelala
chini na kutafuta majibu, sisi wasaidizi wake ametupa kazi ya kutatua
kero za wananchi, hivi ndivyo tunavyozitatua kwa vitendo” Alisema Mhe. Makonda.
Aidha Makonda amesema wodi hiyo itazidisha upatikanaji mzuri wa
huduma bora za Afya kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam huku akieleza
kuwa lengo lake ni kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa mkoa unaotoa huduma
bora za Afya.
“Kama mnakumbuka wakati tunakuja wodi ilivyokuwa
ikitumika akinamama walikuwa wakilundikana chini na wengine wanatumia
kitanda kimoja zaidi ya watatu hadi wanne na wakati mwingine walikuwa
wakilazimika kurudi nyumbani kabla ya muda wa madaktari kuruhusu
kutokana na mazingira duni yaliyokuwa yakikabili wodi hiyo, lakini wodi
hii itamaliza kero hiyo” Aliongeza R.C Makonda.
Hata hivyo Makonda amewataka wadau wa maendeleo wenye dhamira ya
kuchangia shughuli za Maendeleo kwenye Mkoa wa Dar es salaam kujitokeza
kwa wingi Ofisini kwake na Ofisi za Wilaya kuungana na Serikali kuujenga
Mkoa huo.
Post a Comment