Pacha walioungana wafaulu kidato cha sita Tanzania
Pacha walioungana, Maria na
Consolata wamejawa na furaha baada ya kufaulu mitihani yao ya mwisho ya
kidato cha sita, katika shule ya Sekondari ya Udzungwa mjini Iringa,
Kusini magharibi mwa Tanzania.
Maria na Consolata, walio na umri
wa miaka 19, wamefaulu kwa kupata daraja la pili katika masomo yao ya
kidato cha sita na kuwa na matumaini kuwa ndoto yao ya kuwa walimu hapo
baadaye inaelekea kutimia.
Maria na Consolata wameieleza BBC furaha yao:
"Tulipokea
matokeo yetu tukiwa kwenye mazingira ya nyumbani tu, tukiendelea na
shughuli zetu za kila siku, tukaambiwa matokeo yametoka na tumefanya
vizuri, tulikuwa tukiwaza kabla ya hapo, unajua kwenye mitihani ya
mwisho huwezi kujiamini sana," ameeleza Consolata.
Mabinti hawa wangependa kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani humo.
Wameeleza sababu za kuchagua chuo kwenye mkoa wanaoishi tofauti
na vyuo vingine au kama ilivyo kwa wanafunzi wengine ambao wangependa
kubadili mazingira.
"Kwanza tunapenda mazingira ya Iringa,
hatukutaka kwenda Dar es Salaam kwa sababu ya kwanza tunapenda kuishi
pamoja na walezi wetu Masista waliokuwa wanatulea tukiwa wadogo na pili
mikoa mingine ni mbali na tunapoishi. Pia ni kwa sababu kwa hali yetu
tulivyo hatumudu kuishi kwenye mazingira ya joto. Mji wa Iringa ni
baridi, hali hii tumeizoea.''
Maria na Consolata wanaona kuwa, hakuna linaloshindikana iwapo wazazi watawajibika ipasavyo kwa watoto wao wenye ulemavu
"Wazazi
washukuru Mungu kupata watoto wenye changamoto kama wao wasione kuwa na
mtoto mlemavu ni laana. Pili wawaone kama watoto wengine na kuwapa
mahitaji yao ya msingi, wawawezeshe, wawapatie nafasi ya kujiendeleza
maana wakiwezeshwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.'
Post a Comment