Kama wewe ni mtumishi wa umma tovuti hii inakuhusu
KISIGINO HABARI
News by mo7news
Ofisi ya Rais –
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendelea kusanifu na
kuboresha Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCIMS) ili uweze
kutumika kutoa taarifa za msingi kwa watumishi wa umma wengi zaidi kwa
lengo la kuleta mabadiliko ya utendaji kazi katika sekta ya umma nchini.
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Angellah J. Kairuki (Mb) amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi
wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni – Kata ya Kawe, jijini
Dar es Salaam.
Mhe. Kairuki
amesema Mfumo wa HCIMS awali ulikuwa unapatikana Ofisi ya Rais–Utumishi
pekee, lakini baadae ukakasimishwa kwa Maafisa Utumishi lakini sasa
lengo ni kuwafikia watumishi wa umma waweze kuona taarifa zao ili kupata
taarifa sahihi na za uhakika katika kanzidata.
Amesema Tovuti ya Watumishi, Watumishi Portal, imeanzishwa maalum ili watumishi wa umma wajisajili kupitia tovuti ya Ofisi ya Rais-Utumishi yenye anuani www.utumishi.go.tz na kuona taarifa zao za msingi.
Waziri Kairuki,
pamoja na hilo, amesema mfumo wa HCIMS umegatuliwa katika Mamlaka za
Serikali za Mitaa hivi sasa ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na
kufanya maamuzi kwa haraka zaidi.
“Kwa kuwa mahitaji
ya watumishi wa umma ni mengi hivyo tumeona ni vema tukakasimu Mfumo
huu na kwa watumishi wa umma katika kada nyingine ili kurahisisha
utendaji kazi na kuleta mabadiliko” Mhe. Kairuki amesema.
Waziri Kairuki
ameongeza kuwa tayari mafunzo kuhusu namna ya kutumia mfumo
yalikwishatolewa kwa Maafisa Elimu na Makatibu wa Afya wapatao 633.
“Tumeamua kuanza
na sekta hizi kwa sababu ni sekta zenye watumishi wa umma wengi zaidi
ukilinganisha na sekta nyingine lakini tutaendelea kugatua mfumo wa
HCIMS ili ufike katika sehemu nyingi zaidi za kutolea huduma (Service Delivery Points).” Mhe. Kairuki ameongeza.
Mhe, Kairuki yuko
katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Dar es Salaam, ambapo leo ni siku
yake ya tano aliyoitumia kukutana na Watendaji na watumishi wa umma wa
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni-Kata ya Kawe.
Lengo la ziara ni
kukutana na watumishi wa umma na kusikiliza malalamiko, ushauri na
changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuweza
kuzifanyia kazi na kuleta mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini.
Post a Comment